| Dk Mathayo aagiza Narco ianze kunenepesha ng’ombe | Send to a friend |
| Monday, 27 June 2011 20:32 |
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo, ameagiza Shirika la Ranchi za Taifa (Narco) kuanzisha kitengo cha mafunzo ya unenepeshaji mifugo kwa wafugaji, ili kuwa na mifugo yenye tija kwenye soko la nje. Dk Mathayo alisema hayo juzi alipokuwa akizindua duka la nyama la Kongwa lililopo ranchi ya Kongwa, Wilaya ya Kongwa nje kidogo ya mji wa Dodoma. Alisema licha ya Tanzania kuwa ya tatu kwa idadi kubwa ya ng'ombe barani Afrika baada ya Sudani na Ethiopia, inauza tani 200 za ng'ombe kati ya milioni 20. "Haiwezekani tuwe na ng'ombe wengi kiasi hicho, halafu tuuze tani 200 tu, idadi ambayo ni ndogo na haibu kuitaja kwa watu, hivyo naagiza kuanzishwa kwa kituo cha kutoa mafunzo jinsi ya kunenepesha mifugo ili tuweze kupata soko kubwa la nje ambalo litatusaidia kunyanyuka,” alisema Dk Mathayo. Alishauri Narco kuomba mikopo kutoka benki nchini kuwekeza katika unenepeshaji mifugo hiyo, ili kufikia lengo walilojiwekea la kuuza idadi kubwa ya mifugo nchi za nje. Katika hatua nyingine, Dk Mathayo aliwataka wafugaji wadogo nchini kufuga mifugo kulingana na ukubwa wa maeneo wanayomiliki. Naye Meneja Mkuu wa Narco, Dk John Mbogoma, aliomba serikali kusaidia changamoto zinazolikumba shirika hilo zikiwamo kutoa ufumbuzi wa uvamizi wa mara kwa mara wa maeneo ya ranchi. Mwisho. |
No comments:
Post a Comment